The Revolutionary Government of Zanzibar
VOCATIONAL TRAINING AUTHORITY

Mamlaka ya Mafunzo ya Amali Zanzibar YashirikiMaadhimisho ya Miaka 30 ya VETA.

Dar es Salaam, 18 Machi 2025 – Mamlaka ya Mafunzo ya Amali Zanzibar imeshiriki katika maadhimisho ya miaka 30 ya Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) tangu kuanzishwa kwake. Maadhimisho haya yamefanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Hayati Julius Kambarage Nyerere (JNICC), jijini Dar es Salaam, yakiwaleta pamoja wadau mbalimbali wa sekta ya elimu na maendeleo.

Hafla hiyo ilifunguliwa rasmi na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa, ambaye alikuwa mgeni rasmi. Katika hotuba yake, Waziri Mkuu alisisitiza umuhimu wa mafunzo ya ufundi stadi katika kukuza uchumi wa nchi, kuongeza ajira kwa vijana, na kuwajengea uwezo wa kujiajiri.


VETA imeendelea kuwa taasisi muhimu katika kutoa mafunzo ya ufundi na ufundi stadi kupitia vyuo vyake vilivyopo katika mikoa na wilaya mbalimbali nchini. Mafunzo haya yanatolewa kwa watu wa rika tofauti kwa lengo la kuwapa ujuzi unaohitajika kwenye soko la ajira.

Kwa kawaida, VETA hutoa:

Mafunzo ya muda mrefu kwa watu wenye elimu kuanzia kidato cha nne na kuendelea.

Mafunzo ya muda mfupi kwa yeyote anayejua kusoma na kuandika, kwa lengo la kuwawezesha kupata ujuzi wa haraka wa kujiajiri au kuajiriwa.

Maadhimisho haya yamehudhuriwa na wageni mbalimbali, wakiwemo viongozi wa serikali, wadau wa sekta ya elimu, na washirika wa maendeleo, wakionesha mshikamano katika kuendeleza sekta ya ufundi stadi. Mamlaka ya Mafunzo ya Amali Zanzibar, ikiwa miongoni mwa washiriki, imeonesha nia ya kuimarisha ushirikiano kati ya taasisi hizo mbili kwa lengo la kuboresha zaidi elimu ya ufundi.

Kauli mbiu ya maadhimisho ya mwaka huu ni “UFUNDI STADI, FURSA KAMA ZOTE”, ikihamasisha vijana na wananchi kwa ujumla kutumia mafunzo ya ufundi kama njia ya kujenga maisha bora na kuchangia maendeleo ya taifa.

Ushiriki wa Mamlaka ya Mafunzo ya Amali Zanzibar katika maadhimisho haya ni ishara ya mshikamano na dhamira ya pamoja ya kuboresha sekta ya ufundi stadi nchini. Kwa ushirikiano wa taasisi za elimu, serikali, na wadau wa maendeleo, mafunzo ya ufundi yanaendelea kuwa chachu ya maendeleo na ajira kwa Watanzania.

Scroll to Top