Mafundi 224 Watunukiwa Vyeti vya Utambuzi
Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali, Mheshimiwa Lela Mohamed Mussa, amewatunuku vyeti mafundi wazoefu 224 waliopitia mfumo wa kujifunza nje ya mafunzo rasmi. Hafla hiyo imefanyika, Machi 19, 2025, katika Chuo cha Mafunzo ya Amali Vitongoji, Pemba.
Akizungumza wakati wa hafla hiyo, Waziri Lela amewapongeza mafundi hao kwa juhudi zao na mchango wao katika jamii kupitia kazi zao za kila siku. Ameelekeza Mamlaka ya Mafunzo ya Amali (MMA) kutoa barua kwa Wizara ya Kazi pamoja na wakandarasi ili wahitimu wa Mfumo wa Kutathmini Ujuzi (Recognition of Prior Learning – RPL) waweze kushirikiana na wataalamu katika sekta mbalimbali.
Aidha, Waziri ameitaka MMA kuendelea na utaratibu wa kuwatathmini mafundi na kuwapatia vyeti bila urasimu, huku akisisitiza umuhimu wa gharama nafuu ili kuwahamasisha mafundi wengi zaidi kushiriki katika zoezi hilo.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa MMA, Dkt. Bakari Ali Silima, amepongeza wahitimu kwa hatua waliyofikia, akifafanua kuwa RPL hii ni ya pili kwa Pemba na ni mahafali ya tatu kitaifa. Ameeleza kuwa mfumo huu umeleta mafanikio makubwa, ikiwa ni pamoja na kuandaliwa kwa muongozo wa Mafunzo ya RPL unaoweza kutumiwa na vyuo vyote vya VTC.
Dkt. Bakari pia amebainisha kuwa mafanikio ya RPL yameifanya Zanzibar kuwa kitovu cha mafunzo haya, hadi kufikia hatua ya nchi kama Ethiopia na Malawi kuja kujifunza mfumo huu kupitia Shirika la Kazi Duniani (ILO).
Amehitimisha kwa kusisitiza kuwa maisha bora yanategemea huduma bora, ambazo hutolewa na wataalamu wenye vyeti vinavyotambulika rasmi na serikali. Vyeti walivyopata mafundi hao vitawasaidia kupata leseni rasmi za utoaji huduma katika jamii.
Kwa msingi huo, MMA imewahimiza mafundi wengine wazoefu kujitokeza na kujiandikisha katika vyuo vya Mafunzo ya Amali ili kufanyiwa tathmini na kupata vyeti rasmi vya utambuzi wa ujuzi wao.