The Revolutionary Government of Zanzibar
VOCATIONAL TRAINING AUTHORITY

ZANZIBAR YAZINDUA ZANZIBAR STARTUP ASSOCIATION KWA AJILI YA KUIBUA UBUNIFU WA VIJANA.

Zanzibar, 17 Aprili 2025 – Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Mafunzo ya Amali Zanzibar, Dkt. Bakari Ali Silima, amemuwakilisha Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar, Mhe. Khamis Abdulla Said, katika hafla ya uzinduzi wa taasisi mpya isiyo ya kiserikali (NGO) ya Zanzibar Startup Association, inayoongozwa na Ndugu Ikram Ramadhan Soraga.

Uzinduzi huo umefanyika leo katika Ukumbi wa Radio Zanzibar, Rahaleo, Mjini Unguja, ukiwa na lengo la kuwapa vijana nafasi ya kujieleza, kushirikiana, na kuibua mawazo ya kibunifu yatakayosaidia kubadilisha jamii.

Hafla hiyo pia ilihudhuriwa na Afisa Mwandamizi kutoka Shirika la Mawasiliano Zanzibar (ZICTIA), Ndg. Mohd Msoma, pamoja na Dkt. Abubakari Diwani Bakari kutoka Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA).

Katika hotuba yake, Dkt. Bakari Ali Silima alieleza kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inaendelea kutumia juhudi kubwa katika kuboresha miundombinu ya mawasiliano, ikiwa ni moja ya njia za kukuza ubunifu na elimu ya kisasa kwa vijana.

“Tunatambua kuwa mawasiliano bora ni kiungo muhimu kwa elimu ya kisasa, upatikanaji wa taarifa, ujasiriamali wa kidigitali, na hata huduma za kijamii,” alisema Dkt. Bakari. Aliongeza kuwa serikali kwa kushirikiana na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inawekeza kwa kiwango kikubwa katika upanuzi wa mtandao wa intaneti, ujenzi wa minara ya mawasiliano vijijini, pamoja na kuongeza upatikanaji wa vifaa vya TEHAMA katika shule na taasisi za elimu.

Katika mjadala ulioendelea baada ya uzinduzi huo, vijana walipata fursa ya kutoa mawazo yao ya kibunifu na kujadili jinsi miundombinu ya mawasiliano inaweza kusaidia kutatua changamoto zinazowakabili katika jamii. Dkt. Bakari alisisitiza kuwa vijana wana nafasi kubwa sana ya kuleta mabadiliko kupitia matumizi ya teknolojia.

Kwa upande wake, Dkt. Abubakari Diwani Bakari kutoka SUZA aliwasilisha rasmi mpango wa University Roadshow kuelekea Wiki ya Ubunifu Tanzania 2025. Alieleza kuwa lengo kuu la kampeni hiyo ni kuwawezesha wanafunzi, wajasiriamali, na wabunifu kote nchini kushiriki, kujifunza, na kuonyesha vipaji vyao. Pia, vijana watapata ushauri wa moja kwa moja kupitia mentoring sessions zitakazowashirikisha wataalamu kutoka sekta mbalimbali kama teknolojia, biashara, fedha na sera za umma.

Wiki ya Ubunifu Tanzania 2025 inalenga kuonesha kila ambacho vijana, taasisi, na sekta binafsi wanaweza kufanya kwa kutumia ubunifu wao katika kukuza maendeleo ya Taifa, ikiwa na kaulimbiu isemayo “Unlocking Youth Innovation.”

Katika kumalizia hotuba yake, Dkt. Bakari alitoa wito kwa vijana kuhakikisha wanaelimika kuhusu namna ya kulinda haki miliki za ubunifu wao. “Ubunifu ni utajiri; unaweza kumfaidisha mtu kwa kiasi kikubwa kupitia mawazo yake mwenyewe,” alisema. Alitoa rai kwa taasisi mbalimbali kuthamini juhudi za ubunifu zinazofanywa na vijana na wafanyakazi kutoka sekta mbalimbali, ili kuibua wataalamu wenye uwezo wa kubuni mambo mapya kwa ajili ya maendeleo ya taifa kwa ujumla.

Scroll to Top