The Revolutionary Government of Zanzibar
VOCATIONAL TRAINING AUTHORITY

MAADHIMISHO YA MEI MOSI 2025 YAFANA ZANZIBAR – MAMLAKA YA MAFUNZO YA AMALI YANG’ARA KATIKA MAONESHO

Kizimkazi, Zanzibar – Alhamisi, Mei 1, 2025: Zanzibar leo imeadhimisha kwa mafanikio makubwa Siku ya Wafanyakazi Duniani, Mei Mosi, katika viwanja vya Kizimkazi Dimbanii. Maadhimisho hayo yaliyoandaliwa na Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Zanzibar (ZATUC), yamehudhuriwa na viongozi mbalimbali, taasisi za serikali na zisizo za kiserikali, pamoja na mamia ya wafanyakazi kutoka sehemu tofauti za visiwa vya Unguja na Pemba.

Mgeni rasmi katika hafla hiyo alikuwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi, ambaye alipata nafasi ya kutembelea mabanda ya maonesho yaliyoandaliwa na taasisi mbalimbali, yakionyesha kazi na mafanikio ya wafanyakazi wa sekta tofauti.

Miongoni mwa mabanda yaliyovutia ni Banda la Mamlaka ya Mafunzo ya Amali Zanzibar. Ambapo Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka hiyo, Dkt. Bakari Ali Silima, alitoa maelezo kwa Rais juu ya jitihada na ubunifu unaofanywa katika vyuo vya Amali Zanzibar, ambapo wanafunzi wanapokea mafunzo ya fani mbalimbali zenye kuendana na mahitaji ya soko la ajira.

Mamlaka ya Mafunzo ya Amali Zanzibar ilishiriki kikamilifu katika maonesho hayo kupitia vyuo vyake vya Mwanakwerekwe, Mkokotoni na Makunduchi. Maonesho hayo yalihusisha fani kadhaa zikiwemo useremala, ushoni, umeme, na uhandisi wa magari (mechanics). VTA pia imeshiriki katika maonesho kupitia gari linaloonesha kazi na huduma mbali mbali za VTA. ambapo yaliondaliwa na Chuo cha Amali Mwanakwerekwe kilisimama imara kikiongozwa na Mwalimu Mkuu Msaidizi wa chuo hicho, Ndugu Juma Mohd Kesi, ambapo wanafunzi walionesha ubunifu mkubwa katika fani za umeme, elektroniki, useremala na ushoni.

Baada ya kutembelea mabanda, Rais Mwinyi alipokea maandamano rasmi ya wafanyakazi kutoka taasisi mbalimbali, akiwapongeza kwa mchango wao mkubwa katika maendeleo ya taifa. Rais alisisitiza dhamira ya serikali katika kuboresha mazingira ya kazi na kuinua ustawi wa wafanyakazi pamoja na kuwawezesha vijana kupitia elimu ya ufundi na mafunzo ya amali.

Kauli mbiu ya maadhimisho haya ni: “Wafanyakazi Tufanye kazi Kwa Bidii na Nidhamu, Tudai Haki Kwa mujibu wa sheria na tushiriki katika uchaguzi mkuu Kwa Amani.” Ujumbe huu unaonesha mshikamano, ubunifu na kuimarisha ustawi wa wafanyakazi visiwani Zanzibar.

Scroll to Top