The Revolutionary Government of Zanzibar
VOCATIONAL TRAINING AUTHORITY

Mahafali ya Kumi na Mbili(12) Chuo cha Mafunzo ya Amali Mkokotoni.

Serikali ya Mapinduzi Zanzibar inatoa fursa kwa vijana ambao wamehitimu Mafunzo ya Amali kwa kuwapa vipaumbele katika Utekelezaji wa Miradi mbalimbali ya Serikali kwa kutumia utaalamu wao waliopata katika kuleta Maendeleo ya nchi.

Ameyasema hayo Katibu Mkuu Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Ndugu Khamis Abdalla Said wakati akiwatunuku vyeti wahitimu wa Mafunzo ya Amali katika Chuo cha Mafunzo amali Mkokotoni, wilaya ya Kaskazini A Mkoa wa Kaskazini Unguja.

Amesema Serikali inatumbua kuwa kijana mwenye ujuzi ndio injini ya kuwezesha Zanzibar kusonga mbele na kupata maendeleo kwani elimu ya amali ni msingi wa maendeleo ya taifa.

“Serikali imekua ikiwaunga mkono kwa kuwapatia mikopo kupitia wakala wa uwezeshaji wananchi kiuchumi ZEEA ambayo itawasaidia kuendesha miradi yenu kwa ufanisi”

Amesema amevutiwa na kazi mbalimbali zinazofanywa na wanafunzi chuoni hapo kutokana na ubunifu walioonesha ambao unaibuwa vipaji mbalimbali katika kusaidia kukuza teknolojia na kuweza kukuza uchumi wa taifa.

Amesema Wizara itatatua tatizo la uhaba wa vitabu kwa kuanzisha maktaba ya kidigitali ili kuweza kuendana na mafunzo wanayopatiwa kupitia kompyuta kwa kushirikiana na bodi ya huduma za maktaba.

Ameongeza kuwa, Serikali ya Mapinduzi Zanzibar itajenga dakhalia ya wanafunzi katika chuo hicho kwa lengo la kuondosha changamoto ya wanafunzi kutoka masafa marefu na kuweza kusoma kwa ufanisi.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Mafunzo ya Amali Zanzibar Dkt Bakari Ali Silima amewataka wahitimu hao kujiendeleza kimasomo ili kujiongezea nafasi katika soko la ajira hasa katika wakati huu wa mageuzi ya elimu nchini.

“Kwa sasa Wizara ya Elimu ina mpango wa kusomesha mafunzo ya amali katika shule za msingi hivyo ni fursa kwa wahitimu hao kujiendeleza ili kuja kujipatia fursa hii”.

Aidha, Katibu Khamis ametoa wito kwa taasisi za Serikali kutumia huduma zinazotolewa na wanafunzi wa vyuo vya Amaali ikiwemo kufanya marekibisho ya magari ya serikali, pamoja na huduma nyenginezo.

Kwa upande wake, Mkurugenzi vyuo Mamlaka ya Mafunzo ya Amali amesema, Mamlaka ya Mafunzo ya Amali inafanya kazi ya kuwarasimisha mafundi wasio rasmi ambapo jumla ya mafundi wazoefu 215 tayari wamerasimishwa na kutambulika rasmi.

Akisoma risala ya wanafunzi, mwanafunzi Kadiru Fadhil alisema Wanaishukuru Serikali kwa kuwapatia elimu ambayo inatoa mwanga na muelekeo mzuri wa maisha yao kwani kwa sasa wanaweza kujiajiri pamoja na kuajiriwa.

Jumla ya vijana 215 wamehitimu katika fani tofauti ikiwemo Umeme, Ushoni na Kompyuta ambao wamepatiwa vyeti vya kumaliza masomo yao.

Scroll to Top