The Revolutionary Government of Zanzibar
VOCATIONAL TRAINING AUTHORITY

MAHAFALI YA NNE YA CHUO CHA MAFUNZO YA AMALI DAYA YAFANYIKA PEMBA

 

Mamlaka ya Mafunzo ya Amali Zanzibar (MMA) leo tarehe 8 Juni 2026 imeanza rasmi mahafali ya wahitimu wa mwaka 2025 kwa kufanya Mahafali ya Nne ya Chuo cha Mafunzo ya Amali Daya yaliyofanyika katika Mkoa wa Kaskazini Pemba.

Hafla hiyo ilihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Serikali na wadau wa elimu ya amali, ambapo mgeni rasmi alikuwa Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Pemba, Mheshimiwa Mgeni Khatib Yahya. Viongozi wengine waliohudhuria ni Mkuu wa Wilaya ya Wete, Mheshimiwa Abdallah Rashid Ali, Sheha wa Shehia ya Mtambwe Kusini, Ndugu Othman Ali Khamis, Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Mafunzo ya Amali Zanzibar, Dkt. Bakari Ali Silima, Kaimu Mratibu wa Mamlaka ya Mafunzo ya Amali Zanzibar, Ndugu Biubwa Mohd Mselem, pamoja na Mkuu wa Chuo cha Mafunzo ya Amali Daya, Bi. Saada Ali Hamad.

Akizungumza katika hafla hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Mafunzo ya Amali Zanzibar, Dkt. Bakari Ali Silima, alisema vyuo vya amali vina jukumu muhimu la kutoa elimu ya vitendo inayowawezesha vijana kujiajiri na kuajirika. Alieleza kuwa Mamlaka inaendelea kuimarisha ubora wa mafunzo ili kuhakikisha wahitimu wanakuwa na ujuzi unaokidhi mahitaji ya soko la ajira.

Dkt. Bakari pia aliipongeza Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar chini ya uongozi wa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi, kwa kutenga shilingi bilioni 15 katika bajeti ya mwaka wa fedha 2026/2027 kwa ajili ya kuboresha karakana na miundombinu ya vyuo vya mafunzo ya amali nchini.

Aidha, alisema kuwa utekelezaji wa Dira ya Maendeleo ya Zanzibar 2050 unaelekeza kuwepo kwa Chuo cha Mafunzo ya Amali katika kila wilaya, ambapo Serikali inatarajia kujenga vyuo vipya vya mafunzo ya amali katika maeneo ya Tumbe na Chambani kwa upande wa Pemba.

Kwa upande wake, Mkuu wa Chuo cha Mafunzo ya Amali Daya, Bi. Saada Ali Hamad, alisema jumla ya wanafunzi 189 wamehitimu masomo yao kwa mwaka 2025, wakiwemo wanawake 79 na wanaume 110. Wahitimu hao wametoka katika fani mbalimbali zikiwemo Kilimo, Useremala, Upishi, Umeme wa Magari, Ufundi Magari, Ushoni, Front Office, Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (ICT) pamoja na Uvuvi.

Bi. Saada alieleza kuwa licha ya mafanikio yaliyopatikana, chuo hicho bado kinakabiliwa na changamoto mbalimbali za miundombinu ikiwemo uhaba wa karakana za kujifunzia na ubovu wa barabara ya Kivumoni inayotumiwa na wanafunzi wa fani za Kilimo na Uvuvi wanapokwenda kufanya mazoezi kwa vitendo.

Akihitimisha hafla hiyo, Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Pemba, Mheshimiwa Mgeni Khatib Yahya, alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inaendelea kuwekeza katika kuboresha miundombinu ya elimu nchini, ikiwemo vyuo vya mafunzo ya amali, kwa lengo la kuwawezesha vijana kupata ujuzi utakaowasaidia kujitegemea.

Alisisitiza kuwa wahitimu wanapaswa kutumia maarifa na stadi walizopata kujiajiri na kuanzisha shughuli za uzalishaji mali. Aidha, aliwataka kutumia fursa za mikopo isiyo na riba inayotolewa na Serikali kwa vijana, wanawake na watu wenye ulemavu ili kuendeleza shughuli zao za kiuchumi.

Katika kilele cha hafla hiyo, Mheshimiwa Mgeni Khatib Yahya alitunuku vyeti na zawadi kwa wahitimu pamoja na wanafunzi waliofanya vizuri zaidi katika masomo yao.

Imetolewa na:
Kitengo cha Uhusiano
Mamlaka ya Mafunzo ya Amali Zanzibar.

Scroll to Top