The Revolutionary Government of Zanzibar
VOCATIONAL TRAINING AUTHORITY

MAHAFALI YA 12 YA CHUO CHA MAFUNZO YA AMALI MWANAKWEREKWE YAFANYIKA ZANZIBAR.

Mamlaka ya Mafunzo ya Amali Zanzibar inaendelea na mfululizo wa mahafali ya wahitimu wa mwaka 2025, ambapo leo tarehe 10 Juni 2026, Chuo cha Mafunzo ya Amali Mwanakwerekwe kimefanya Mahafali yake ya 12 yaliyofanyika katika viwanja vya chuo hicho, kilichopo, Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja.

Mgeni rasmi katika mahafali hayo alikuwa Naibu Katibu Mkuu wa Utawala, Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar, Ndugu Amos John Henock, ambaye aliwapongeza wahitimu kwa juhudi walizozionesha katika kipindi chote cha masomo yao na kuwataka kutumia elimu na ujuzi walioupata kujiletea maendeleo binafsi na ya jamii kwa ujumla.

Akizungumza katika hafla hiyo, Ndugu Amos alisema kuwa mafunzo ya amali ni miongoni mwa njia muhimu za kuwawezesha vijana kupata ajira za moja kwa moja kupitia kujiajiri au kuajiriwa katika sekta mbalimbali za uzalishaji na huduma. Alieleza kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inaendelea kuthamini mchango wa mafunzo ya amali katika kukuza uchumi wa nchi na kupunguza tatizo la ukosefu wa ajira kwa vijana.

Aidha, alisema serikali inatarajia kujenga vyuo sita vipya vya mafunzo ya amali katika mikoa ya Unguja na Pemba ili kuongeza fursa za upatikanaji wa elimu ya ufundi na ujuzi kwa vijana wengi zaidi.

Pia aliwahamasisha wahitimu kutumia fursa ya mikopo isiyo na riba inayotolewa na serikali na taasisi mbalimbali kwa ajili ya kuendeleza taaluma zao, kuanzisha miradi ya kiuchumi na kujikwamua kiuchumi.

Baada ya hotuba yake, Ndugu Amos aliwatunuku stashahada na vyeti wahitimu wa mwaka 2025 waliomaliza masomo yao katika fani za Ushoni, Useremala, Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA), Elektroniki pamoja na Umeme.

Awali, Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Mafunzo ya Amali Zanzibar, Dkt. Bakari Ali Silima, alimshukuru mgeni rasmi kwa kukubali kushiriki katika mahafali hayo na kuendelea kuunga mkono juhudi za serikali za kuimarisha mafunzo ya amali nchini.

Dkt. Silima pia ameiyomba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia miradi ya maendeleo ya Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali kwa mwaka wa fedha 2027/2028 kujenga jengo la ghorofa katika Chuo cha Mafunzo ya Amali Mwanakwerekwe ili kuongeza karakana ,madarasa ya kujifunzia kutokana na kuongezeka kwa mahitaji ya mafunzo hayo.

Sambamba na hilo, Dkt. Silima alisema Mamlaka inaendelea kuhimiza ubunifu katika vyuo vyake, ambapo katika Mahafali ya Chuo cha Mafunzo ya Amali Mkokotoni yatakayofanyika tarehe 12 Juni 2026, walimu waliofanya ubunifu wa kipekee katika ufundishaji na mafunzo watatunukiwa zawadi maalum kwa lengo la kuongeza hamasa na kuendeleza ubunifu wa kitaaluma katika vyuo vya mafunzo ya amali.

Jumla ya wahitimu 134 wamehitimu masomo yao kwa mwaka 2025, ambapo 66 ni wanawake na 68 ni wanaume.

Imetolewa na:
Kitengo cha Uhusiano
Mamlaka ya Mafunzo ya Amali Zanzibar.

Scroll to Top