The Revolutionary Government of Zanzibar
VOCATIONAL TRAINING AUTHORITY

Naibu Waziri wa Wizara ya Elimu Mafunzo ya Amali Zanzibar Aitaka Mamlaka ya Mafunzo ya Amali Zanzibar Kuongeza Kasi ya Ubunifu na Uwajibikaji.

Zanzibar, 4 Februari 2026
Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Mafunzo ya Amali Zanzibar (VTA), Dkt. Bakari Ali Silima, leo amepokea ugeni kutoka Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar ulioongozwa na Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali.Mheshimiwa Khadija Salum Ali, pamoja na Naibu Katibu Mkuu (Utalawa), Ndugu Amos John Henock.

Ugeni huo umefanya ziara katika ofisi za Mamlaka hiyo zilizopo Malindi, Zanzibar, ukiwa na lengo la kujitambulisha pamoja na kusikiliza changamoto mbalimbali zinazozikabili taasisi zilizo chini ya Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar, ili kuona namna bora ya kuboresha upatikanaji na utoaji wa elimu nchini.

Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Mheshimiwa Khadija Salum Ali amewataka wafanyakazi wa Mamlaka ya Mafunzo ya Amali Zanzibar kuongeza kasi ya ubunifu, uwajibikaji na ufanisi katika utoaji wa huduma kwa jamii, ili kuchangia maendeleo ya taifa na jamii kwa ujumla.

Aidha, Mheshimiwa Khadija alipongeza juhudi zinazofanywa na VTA katika kuongeza nafasi za ajira kwa vijana kupitia elimu ya ufundi na ubunifu, jambo linalosaidia kupunguza utegemezi wa ajira za serikali pekee. Pia aliwasisitiza wafanyakazi kuzingatia sheria za kazi na utumishi wa umma, kuacha kufanya kazi kwa mazoea na kuhakikisha wanatekeleza majukumu yao kwa weledi.

Vilevile, amesisitiza umuhimu wa kutekeleza Ilani ya Chama cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka 2025/2030 ili kufikia malengo yaliyopangwa na Serikali katika sekta ya elimu na mafunzo ya amali.

Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu (Utalawa), Ndugu Amos John Henock, amesema kuwa ushirikiano miongoni mwa wafanyakazi ni msingi muhimu wa kuongeza ufanisi kazini. Alionya kuwa migogoro, chuki na kutoelewana kazini huathiri maendeleo ya taasisi, na kuwataka wafanyakazi kuimarisha mshikamano na ubunifu ili kuongeza upatikanaji wa ajira za kujitegemea.

Akitoa maelezo ya changamoto zinazokabili Mamlaka, Mkurugenzi Mtendaji wa VTA, Dkt. Bakari Ali Silima, amesema Mamlaka inakabiliwa na changamoto kadhaa ikiwemo ukosefu wa fedha za SDL.

Hata hivyo, pamoja na changamoto hiyo,amesema VTA imepata mafanikio makubwa ikiwemo kuwapatia wanafunzi ujuzi unaowawezesha kujiajiri na kubuni bila kutegemea ajira za serikali. Pia Mamlaka imefanikiwa kusajili vyuo vya amali 63, vikiwemo vya sekta binafsi.

Alisisitiza kuwa VTA ina jukumu la kusimamia, kusajili na kutoa miongozo kwa vyuo vya amali nchini ili kuhakikisha ubora wa mafunzo yanayotolewa.

Naye Mkurugenzi wa Rasilimali Watu, Utawala na Mipango wa VTA, Ndugu Patima Khamis Rajabu, aliwashukuru viongozi hao kwa ziara yao na kuipongeza Wizara ya Elimu Zanzibar kwa juhudi zake za kuhakikisha Sera ya Elimu inaendana na kasi ya dunia, kwa lengo la kuwazalisha wahitimu wenye ujuzi na ubunifu katika sekta mbalimbali.

 

 

Scroll to Top