MAHAFALI YA 13 YA CHUO CHA MAFUNZO YA AMALI MKOKOTONI YAHITIMISHA MFULULIZO WA MAHAFALI YA MMA ZANZIBAR.

Mamlaka ya Mafunzo ya Amali Zanzibar leo tarehe 12 Juni 2026 imehitimisha rasmi mfululizo wa mahafali ya wahitimu wa mwaka 2025 yaliyokuwa yakifanyika kuanzia tarehe 8 Juni 2026 katika vyuo vyake vya Unguja na Pemba, kwa kufanya Mahafali ya 13 ya Chuo cha Mafunzo ya Amali Mkokotoni.
Mahafali hayo yamefanyika katika viwanja vya Chuo cha Mafunzo ya Amali Mkokotoni, Mkoa wa Kaskazini Unguja, ambapo Mgeni Rasmi alikuwa Mstahiki Meya wa Manispaa ya Wilaya ya Kaskazini A, Mheshimiwa Nyange Kheir Ali.
Akizungumza katika hafla hiyo, Mheshimiwa Nyange Kheir Ali amepongeza juhudi zinazofanywa na Mamlaka ya Mafunzo ya Amali Zanzibar katika kuwawezesha vijana kupata ujuzi wa kazi na kujiajiri.
Amesema mafunzo yanayotolewa na vyuo vya mamlaka hiyo yana mchango mkubwa katika kuimarisha maendeleo ya kiuchumi na kijamii nchini.
Aidha, ameahidi kushirikiana na viongozi mbalimbali wa Jimbo la Tumbatu pamoja na wadau wengine katika kutafuta ufumbuzi wa changamoto zinazoikabili Chuo cha Mafunzo ya Amali Mkokotoni, ikiwemo ukosefu wa barabara za ndani ya chuo, changamoto ya dahalia pamoja na changamoto nyingine za miundombinu na mazingira ya kujifunzia.
Katika mahafali hayo, Mheshimiwa Nyange Kheir Ali aliwatunuku Astashahada wahitimu wa fani mbalimbali zikiwemo Upishi, Utembezaji Watalii, Kilimo cha Mboga Mboga, Ushonaji pamoja na fani nyingine zinazotolewa chuoni hapo.
Awali, Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Mafunzo ya Amali Zanzibar, Dkt. Bakari Ali Silima, aliwasilisha taarifa ya chuo ambapo alieleza mafanikio yaliyopatikana pamoja na changamoto zinazoendelea kufanyiwa kazi ili kuboresha utoaji wa mafunzo na mazingira ya kujifunzia.
Katika hafla hiyo, Mgeni Rasmi pia aliwatunuku vyeti vya ubora walimu na wanafunzi waliofanya vizuri katika taaluma, nidhamu na ubunifu wa kazi mbalimbali.
Mahafali ya Chuo cha Mafunzo ya Amali Mkokotoni yamehitimisha rasmi mfululizo wa mahafali ya mwaka 2025 ya Mamlaka ya Mafunzo ya Amali Zanzibar yaliyofanyika katika vyuo vya Unguja na Pemba kuanzia tarehe 8 hadi 12 Juni 2026.
Imetolewa na:
Kitengo cha Uhusiano
Mamlaka ya Mafunzo ya Amali Zanzibar.