The Revolutionary Government of Zanzibar
VOCATIONAL TRAINING AUTHORITY

MAHAFALI YA TATU YA CHUO CHA MAFUNZO YA AMALI MAKUNDUCHI YAFANYIKA UNGUJA

Mamlaka ya Mafunzo ya Amali Zanzibar (MMA) kupitia Chuo cha Mafunzo ya Amali Makunduchi leo imefanya Mahafali ya Tatu ya wahitimu wa mwaka 2025 yaliyofanyika katika viwanja vya chuo hicho, Mkoa wa Kusini Unguja.

Mgeni rasmi katika mahafali hayo alikuwa Naibu Katibu Mkuu Taaluma wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali, Dkt. Mwanahamisi Adam Ameir, ambaye aliwataka wahitimu kutumia ujuzi walioupata kujiajiri na kuajiriwa, huku wakidumisha nidhamu, ubunifu na kuendelea kujiendeleza kitaaluma ili kuchangia maendeleo ya jamii na taifa.

Dkt. Mwanahamisi pia amepongeza juhudi za Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Mafunzo ya Amali Zanzibar, Dkt. Bakari Ali Silima, katika kuimarisha vyuo vya mafunzo ya amali na kuongeza ubora wa mafunzo yanayotolewa.

Katika mahafali hayo, wahitimu walitunukiwa vyeti na stashahada katika fani mbalimbali zikiwemo Ufundi Umeme wa Majumbani na Viwandani, Uhunzi, Uvuvi, Ushonaji, Uongozaji Wageni, Upishi pamoja na Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (ICT).

Kwa upande wake, Dkt. Bakari Ali Silima amesema Mamlaka inaendelea kuviwezesha vyuo vya mafunzo ya amali kutoa elimu inayokidhi mahitaji ya soko la ajira na maendeleo ya teknolojia. Ameeleza kuwa Chuo cha Mafunzo ya Amali Makunduchi kimeendelea kufanya vizuri katika mashindano mbalimbali ikiwemo michezo ya Kabaddi na Mashindano ya Kitaifa ya Ujuzi Tanzania 2026.

Naye Mkurugenzi wa Vyuo na Mafunzo wa MMA, Mhandisi Abdallah Mohammed Hambal, ameishukuru taasisi ya Mwanamke Initiative Foundation kwa kufadhili wahitimu wa mafunzo ya muda mfupi katika fani za ushonaji na upishi, huku akiomba kusaidiwa uwekaji wa mfumo wa umeme wa jua chuoni ili kuimarisha upatikanaji wa umeme wa uhakika.

Imetolewa na:
Kitengo cha Uhusiano
Mamlaka ya Mafunzo ya Amali Zanzibar.

Scroll to Top